Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini upotevu wa mabilioni ya walipa kodi kwenye manunuzi ya umma yaliyofanywa na taasisi za serikali bila kuzingatia sheria na taratibu husika.
Ripoti hiyo ya Mwaka wa Fedha 2015/16 iliyotolewa wiki iliyopita na CAG, Profesa Mussa Assad imebaini mapungufu mengi katika usimamizi wa mikataba na miradi ikitaja kwa sampuli mikataba nane ya miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 63 na shilingi trilioni 2.2 ambayo haikusimamiwa ipasavyo.
Aidha, CAG alibaini kuwepo kwa manunuzi ya bidhaa na huduma zenye thamani ya shilingi bilioni 23.98 ambayo yalifanywa na taasisi za umma bila kutumia njia ya ushindani, kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma.
“Nilibaini kuwepo kwa ucheleweshaji wa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 23.32… kwa idara za wizara mbalimbali na Wakala walifanya manunuzi ya bidhaa na huduma za shilingi bilioni 2.48 bila kupata idhidi ya Bodi ya Zabuni,” alisema CAG.
Ukaguzi huo ulibaini pia kuwepo kwa matumizi ya shilingi bilioni 11.253 bila kuwa na mikataba aua makubaliano sahihi kati ya taasisi nunuzi na wazabuni, kinyume cha kifungu cha 10(4) cha Kanuni za Manunuzi ya Umma za mwaka 2013.
Ripoti ya mkaguzi iliotoa mfano wa Wizaa ya Maji na Umwagiliaji ambayo iliingia mkataba wenye thamani ya shilingi milioni 491.047 na kampuni ya International Company kwa ajili ya kusambaza maji katika eneo la Gidahababeing hadi Hanang, bila mkataba huo kukaguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2011 iliyotaka mkataba unaozidi shilingi milioni 50 kukaguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kadhalika, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliingia mkataba wa shilingi milioni 668 ambao haukupitiwa na kukaguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Hayo ni baadhi ya mapungufu katika usimamizi wa mikataba ya manunuzi ya umma uliofanywa na taasisi mbalimbali za umma na kupelekea kupotea kwa kiasi kikubwa cha fedha za walipakodi, uliobainika kupitia Ripoti hiyo ya CAG.