Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imetumia Sh. 2.58 bilioni bila kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume cha utaratibu.
Hayo yamebainishwa kupitia ripoti ya CAG ya ukaguzi unaoishia Juni 30, 2019 ambapo ameeleza kuwa fedha hizo zilitumika kuanzisha channel ya runinga ya ‘Utalii Festival’ na kampeni yake kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, CAG ameeleza kuwa wakati wa ufuatiliaji, alijulishwa kuwa kiasi hicho cha fedha kilikusanywa kutoka katika mafungu mengine ya Wizara pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kama TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), TAFSA na Tawa.
CAG amesema alibaini kuwa fedha hizo zilipitishwa na Menejimenti ya Wizara hiyo kupitia vikao mbalimbali.
“Nilijulishwa kuwa bajeti ya ‘Urithi Festival’ ilipitishwa na Menejimenti ya Wizara kupitia vikao mbalimbali,” alisema CAG.
Urithi Festival ilizinduliwa rasmi Septemba 2018, lengo likiwa kutangaza vivutio vya utalii na urithi wa asili.