Msajili wa Hazina (TR), Lawrence Mafuru na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad  wametofautiana kuhusu umiliki wa Shirika la Promotion of Rural Initiatives and Development Enterprises (PRIDE).

Wakati ripoti ya CAG ya mwaka huu ikiendelea ikieleza kama ilivyo katika ripoti ya mwaka 2013/2014 kuwa PRIDE ni shirika la Umma, TR amesema kuwa ofisi yake haina nyaraka zozote zinazoonesha kuwa shirika hilo linamilikiwa na umma.

Katika maelezo yake, CAG ameeleza kuwa PRIDE ilianzishwa chini ya Mei 5, 1993 chini ya Sheria ya Makampuni (CAP 212) kwa lengo la kutoa mikopo midogo kwa wajasiriamali, na kwamba fedha za kulianzisha shirika hilo zilizotolewa na serikali ya Norway kwa makubaliano na Tanzania, kabla ya Sweden kujiunga kusaidia Shirika hilo mwaka 2001.

CAG ameeleza kuwa kufikia mwaka 2008, hisa zote za PRIDE zilikuwa zinamilikiwa na Serikali, lakini shirika hilo liliondolewa kwenye orodha ya mashirika ya umma katika ofisi ya TR baada ya Juni 30 mwaka 2008. Ripoti hiyo imeeleza kuwa sababu za kuliondoa shirika hilo kwenye orodha ya mashirika ya umma kwenye ofisi ya TR hazikubainika.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, kila Shirika la Umma linatakiwa kuleta hesabu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya kukaguliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kumalizika kwa mwaka wa fedha. Hata hivyo, hesabu za Pride Tanzania hazijawahi kuwasilishwa kwenye ofisi yangu kwa ajili ya ukaguzi kama inavyotakiwa na sheria,” inaeleza ripoti ya CAG.

Ingawa TR amekubaliana na CAG kuhusu uanzishwaji wa shirika hilo kwa mujibu wa sheria, amesisitiza kuwa hakuna nyaraka ofisini kwake zinazoonesha kuwa ni shirika la umma.

“Serikali inaweza kuanzisha kampuni kwa kuhamisha mtaji; mlipaji ambaye ni Serikali atapeleka kiasi cha fedha kwa shirika lililoanzishwa cha Sh100 bilioni kupitia Benki ya Uwekezaji nchini (TIB),” alisema TR.

Alieleza kuwa Serikali imekuwa ikianzisha mashirika kwa matamko yake kama vile Brela, Ewura, TCRA yanakuwa ya umma pamoja na mashirika yaliyoanzishwa na sheria za Bunge.

“Lakini Serikali haikuweka mtaji PRIDE wala haikutamka, ndiyo maana kwenye ofisi hii (Msajili wa Hazina) hakuna kumbukumbu yoyote,” alisisitiza.

Claudio Ranieri: Nitakua Wa Mwisho Kufahamu Matokeo
Hassan Shehata Kujitwisha Mgizo Wa Zamalek Sports Club