Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad amesema kuna haja ya kuanza na safu mpya ya viongozi serikalini, kwa kile alichokidai kuwa waliopo wengi hawana uwezo mzuri kiutendaji.

Profesa Assad amesema hayo leo Aprili 10, 2021 wakati wa uzinduzi wa mfululizo wa midahalo kwa umma itakayokuwa ikiandaliwa na Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM).

Amesema kwa mtazamo wake asilimia 60 au 50 ya viongozi ndani ya Serikali sio wazuri, hivyo wanapaswa kupumzishwa ili mambo yaanze upya.

“Viongozi wengi sio wazuri au hawakidhi kiwango kinachohitajika, tatizo langu ni moja tu inapofika mahali unaona mtu anakosea na huwezi kusema kama mtu anakosea, unakuwa umefika mahali pabaya sana, sio lazima umkosoe wazi wazi,  lakini angalau basi andika kwamba mheshimiwa nimeona umefanya jambo hili na hili, lakini nafikiri kimsingi jambo hilo halikuwa sawa,  rai yangu turekebishe hapa na hapa, akipata rai kwa mtu mmoja atakasirika, akipata rai hiyo kwa watu 10 kwenye cabinet (baraza) yake lazima asikilize,” amesema Profesa Assad.

“Ndiyo maana nasema tuanze upya tuanze na hao wachache ambao wanakwenda vizuri, hilo pia ni somo kwamba ambao nao ‘in the future’ (baadaye) watakuwa wa ovyoovyo,  dawa yao ni hiyo ya  kuwaweka kando na kuanza upya,” amesisitiza Profesa Assad.

Aidha, amesema utaratibu wa Bunge likipitia mapendekezo yanaachwa si mzuri hivyo ni lazima kuwepo kwa kanzi data itakayotumiwa na Bunge na Ofisi ya CAG kuhakikisha kuwa mapendekezo yanayotolewa katika ukaguzi wa hesabu za serikali yanafanyiwa kazi.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 11, 2021
Wanawake wajawazito wahanga wa harufu mbaya kinywani