Kiungo wa Brighton, Moises Caicedo amefikia uamuzi wa kujiunga na Chelsea na kuikacha Arsenal katika dirisha la usajili wa majira ya Kiangazi licha ya Washika Mtutu hao kuihitaji huduma yake tangu dirisha lililopita la majira ya Baridi.
Taarifa zinadai makubaliano binafsi yameshafanyika na kinachoendelea sasa ni mazungumzo ya mwisho baina ya Chelsea na Brighton juu ya masuala ya ada ya uhamisho ya staa huyo wa kimataifa wa Ecuador.
Caicedo ambaye katika dirisha lililopita alishafanya makubaliano binafsi na Arsenal na akaiomba Brighton imuachie ili atue Emarates kwa sasa amebadilisha uamuzi na anataka kutua Stamford Brigde kutokana na ofa yao.
Brighton ipo tayari kumpiga bei kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21 katika dirisha hili la usajili lakini kwa ofa inayotajwa kuwa ni zaidi ya Pauni 50 milioni.
Mkataba wa sasa wa Caicedo ambaye ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Brighton tangu msimu uliopita, mkataba wake wa sasa unamal- izika mwaka 2027. Msimu uliopita alicheza mechi 43 za michuano yote.
Chelsea ilifanya uamuzi wa haraka kumsajili Caicedo baada ya kushindwa kumsajili kiungo wa Primeira Liga Sporting CP, Manuel Urgarte ambaye amekwenda Paris Saint-Germain.
Hii ni mara ya pili, Chelsea kuipora Arsenal mchezaji, katika dirisha lililopita klabu hiyo iliipora Mykhailo Mudryk. Mudryk alishafanya mazungumzo ya awali na Arsenal akiwa anaitumikia FC Desna Chernihiv lakini katika dakika za mwisho, winga huyo wa Ukraine aliichana na mipango hiyo na kutua darajani.