Mlinda Lango kutoka nchini Brazil Caique Luiz Santos da Purificacao muda wowote kuanzia sasa anaweza kutua katika ardhi ya Tanzania na kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba SC, huku mwenyewe akifunguka.
Inafahamika kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ndiye aliyependekeza jina la Caique akiamini ataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha chake kutokana na ubora alionao akiziba nafasi ya Beno Kakolanya aliyepewa ‘Thank You’, na kutimkia Singida Fountain Gate FC.
Purificaca mwenye umri wa miaka 25, sambamba hilo pia ataziba pengo la Aishi Manula atakayekuwa nje ya uwanja hadi Novemba kutokana na jeraha la nyonga ambalo alifanyiwa upasuaji hivi karibuni Afrika Kusini.
Robertinho wakati anampendekeza Caique aliwasisitizia viongozi wa Simba SC wamlete kwani anamjua vyema kudaka na anaamini ataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kutoa ushindani kwa makipa waliopo kina Manula, Salim Ally na Ahmed Feruzna hapo ndipo vigogo wa timu wakaanza harakati za kumnasa.
“Lazima tusajili kipa. Tunataka kila eneo tuwe na watu zaidi ya wawili wenye ushindani na tayari nimeupa uongozi jina la moja ya makipa ninaowataka (Caique), naamini wanalifanyia kazi,” amesema Robertinho.
Hata hivyo, Mlinda Lango huyo amethibitisha kuwepo kwa dili hilo huku akisisitiza kutua nchini kama kila kitu kitaenda vizuri.
“Ni kweli Simba SC ilinitafuta. Kuna mazungumzo na yamefikia sehemu nzuri. Kila kitu kikienda vizuri, basi nipo tayari kujiunga nao muda wowote kuanzia sasa,” amesema Caique aliyemaliza mkataba na timu ya Ypiranga RS inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.
Pamoja na Yprang, kwa nyakati tofauti Caique aliwahi kuzichezea timu nyingine za Brazil ikiwemo EC Victoria iliyomkuza katika akademi yake na pia CSA.
Pia alicheza nchini Marekani kwenye klabu ya Rochester Sambamba na Cyprus kwenye klabu ya Ermis Aradippou. Caique aliwahi kuichezea timu ya taifa ya vijana ya Brazil wasiozidi umri wa miaka 20 (Brazil U-20) kuanzia 2016 hadi 2018 akiwa kipa namba moja ambako alicheza na mastaa wa sasa dunianai wakiwemo Richarson de Andrade wa Tottenham Hotspur, Eda Miltao wa Real Madrid, Douglas Luiz wa Aston Villa, Lucas Paqueta wa West Ham United na Gabriel Magalhes wa Arsenal.