Benchi la Ufundi la Real Madrid limeingia ubaridi baada ya kiungo wao kutoka Ufaransa Eduardo Camavinga kupata majeraha akiwa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania mwishoni mwa juma dhidi ya Getafe.
Ancelotti na wenzake wameingiwa ubaridi na kuhofia huenda Camavinga akakosa mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Manchester City utakaochezwa Etihad kesho kutwa, Jumatano.
Camavinga alionekana akiweka barafu kwenye goti lake alipokuwa benchi na kuzua hofu kwa Meneja Carlo Ancelotti.
Kiungo huyo kinda alionyesha kiwango bora dhidi ya Man City katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, akicheza kama beki wa pembeni huku akisaidia kupeleka mashambulizi eneo la hatari.
Naye Karim Benzema aliukosa mchezo dhidi ya Getafe uliomalizika kwa ushindi wa bao 1-0 na inaelezwa Mshambuliaji huyo alipumzishwa kwa ajili ya nusu fainali dhidi ya Man City.
Licha ya ushindi wa Madrid dhidi ya Getafe, vijana wa Ancelotti tayari wameshaukosa ubingwa wa La Liga kwani wamepitwa kwa tofauti ya alama 14 na FC Barcelona.