Mabingwa wa Afrika, timu ya taifa ya Cameroon watacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Tunisia (Eagles of Carthage) mwezi ujao.
Cameroon na Tunisia watacheza mchezo wa kirafiki Marchi 24 katika uwanja wa Mustapha Ben Jannet uliopo mjini Monastir nchini Tunisia.
Shirikisho la soka nchini Tunisia, limethibitisha uwepo wa mchezo huo kupitia tovuti yake: “Tumefikia makubaliano ya kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Cameroon utakaochezwa Machi 24 kwenye uwanja wa Mustapha Ben Jannet mjini Monastir.”
Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki, utakiandaa kikosi cha mabingwa hao wa AFCON 2017 kwa ajili ya heka heka za kusaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia ambapo Cameroon watapambana na Nigeria.
Kabla ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Nigeria mwezi Agosti, Cameroon watashiriki michuano ya kombe la mabara itakayofanyika nchini Urusi mwezi Juni.
Kwa upande wa Nigeria wanajiandaa na mchezo huo kwa kujipima nguvu na Senegal na Burkina Faso mwezi ujao.