Bondia Mmexico, Canelo Alvarez ameendeleza ubabe akitetea mkanda wake wa ubingwa wa dunia wa masumbwi uzito wa kati baada ya kumzima Rocky Fielding katika raundi ya tatu, katika pambano lililofanyika usiku wa kuamkia leo nchini Marekani.
Canelo ambaye hivi karibuni alikata mzizi wa fitna kwa kumpiga mbabe Gennady Golovkin (GGG), amekamilisha usemi wa wachambuzi wa masuala ya masumbwi walioeleza kuwa pambano hilo lingekuwa rahisi kwake.
Ushindi huo umeendelea kung’arisha rekodi ya Canelo ambayo sasa inakuwa 51-1-2, 34 KO, ikimuongezea doa Rocky ambaye anakuwa amepoteza mara ya pili pambano lake (27-2, 15 Kos). Mbabe pekee aliyewahi kumpiga Canelo anabaki kuwa ni Floyd Mayweather.
Kumalizika kwa pambano hilo kumechochea zaidi moto wa kufanyika kwa pambano la tatu kati ya Canelo na hasimu wake GGG, ambapo fununu zinaonesha kuwa huenda wakazichapa tena Mei 4 mwakani nchini Marekani.
Lakini zipo tetesi kuwa huenda mbabe Daniel Jacobs ambaye aliwahi kumpa tabu GGG ulingoni ingawa alishindwa pambano, ndiye anayepangwa kuzichapa na Canelo Mei mwakani.
Muda utazungumza yote, tuendelee kusubiri kuona nani atakuwa na nafasi nyingine ya kukutana uso kwa macho ulingoni na Mmexico, Canelo Alvarez.