Gwiji wa soka kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Man Utd, Eric Cantona amevunja ukimya na kuwajibu mashabiki waliokua wakizungumzia kurejea kwake katika medani ya mchezo huo.

Cantona amekua akihusishwa na mpango wa kuajiriwa na klabu ya  Olympique Marseille inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa, kama mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo.

Kwa muda sasa, gwiji huyo anayeendelea kukumbukwa huko Old Trafford kutokana na mazuri aliyoyaonyesha kuanzia mwaka 1992–1997 amekua akizunguzwa juu ya kurejea kwake katika soka katika nyanja ya uongozi.

Alipoulizwa na muandishi wa habari wa moja ya kituo cha televisheni cha nchini kwao Ufaransa kuhusu uvumi huo, Cantona alicheka na kuonyesha uso wa bashasha, lakini hakutoa majibu yaliyoeleweka.

Cantona alisema ni jambo zuri kusikia akizungumzwa na kila mmoja kuhusu kurejea katika medani ya soka kama kiongozi, lakini mwisho alimuuliza muandishi swali ambalo halikupata jibu la haraka.

“Inafurahisha kusikia hivyo, lakini ukweli ni kwamba jambo moja ama lingine lina taratibu zake na wewe kama muandishi mpaka umekuja kuniuliza huenda ukawa umesikia mahala juu ya kurejea kwangu katika soka, kwani wewe unaonaje?” Alihoji Cantona

Hata hivyo mshambuliaji huyo ambaye alikua akivaa jezi namba saba alipokua Man Utd, amesisitiza kwamba soka ni mchezo uliomtengeneza na kutambulika duniani kote na hadhani kama itakua dhambi kwa yoyote atakae mzungumzia kuhusu mchezo huo.

“Soka ni mchezo ulionikuza na kunitengenezea jina langu, sioni sababu ya kuchukizwa na jambo ambalo linaniingiza katika utaratibu wa kuzungumzwa kupitia mkondo huo.”

Cantona aliwahi kuitumikia klabu ya Olympique Marseille kama mchezaji kuanzia mwaka 1988–1991 na kama atarejea klabuni hapo kama kiongozi, atakua amepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kutokana na kuifahamu vyema klabu hiyo ambayo imewahi kutwaa ubingwa wa nchini Ufaransa mara tisa.

Klabu nyingine ambazo Cantona aliwahi kuzitumikia ni Auxerre (1983–1988), Martigues (1985–1986), Bordeaux (1989), Montpellier (1989–1990), Nîmes (1991) pamoja na Leeds United (1992).

Mara baada ya kustaafu soka mwaka 1997, Cantona amekua akijishughulisha na masuala ya kutengeneza matangazo mbalimbali ya kibiashara yanayohusu mchezo wa soka na kwa kipindi kirefu alifanya hivyo akiwa na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike.

 

Pep Guardiola Kuizidi Kete Man utd Kwa Nikola Maksimovic?
Julio: Waamuzi Walichezesha Kwa Maagizo Maalum Ya Kuibeba Yanga