Meneja wa klabu ya SSC Napoli Carlo Ancelotti amesema anakabiliwa na changamoto ya kukipanga kikosi chake, kuelekea kwenye mchezo wa mwishoni mwa juma hili ambao utawakutanisha na mabingwa watetezi wa Serie A, Juventus FC.
Ancelotti amesema umahiri wa wachezaji wote alionao kikosini kwa sasa, ndio sababu kubwa ya kupata changamoto hiyo, kutokana na kuamini kila mmoja ana sifa ya kuwakabili mabingwa hao, ambao watakua nyumbani mwishoni mwa juma hili.
Meneja huyo mkongwe amesema lengo kubwa ni kuhakikisha anapata ushindi ugenini dhidi ya Juventus, ili kuendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kiushindani katika ligi ya nchini Italia, na mpaka sasa hana jibu sahihi la nani ataanza na nani atakua benchi siku hiyo.
“Tupo vizuri, wachezaji wangu wana ari kubwa ya kupambana na yoyote msimu huu, mpaka sasa ninashindwa kutambua nani anapaswa kuwa sehemu ya kikosi mwishoni mwa juma hili,” Alisema Ancelotti alipohojiwa na Sky Sport Italia.
“Baada ya mchezo wetu dhidi ya Parma, tumeanza mandalizi kabambe ya kuwakabili JUventus, na kila mchezaji anaonyesha juhudi kubwa mazoezi, hadi napata wakati mgumu wa kufikiria nani anapaswa kuwa sehemu ya jeshi langu.”
“Mfumo wetu msimu huu, unampa nafasi kila mmoja kuwa tayari kucheza, lakini nina uhakika hadi siku ya ijumaa nitakua nimepata jibu sahihi la kikosi kamili kitakachoanza dhidi ya Juventus.”
SSC Napoli kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya nchini Italia Serie A kwa kufikia lama 15, huku wapinzani wao Juventus wakiongoza msimamo huo kwa kuwa na alama 18.
Endapo SSC Napoli watafanikiwa kuibuka na ushindi mwishoni mwa juma hili, watakuwa sawa na Juventus kileleni, lakini kitakacho zitofautisha timu hizo ni uwiyano wa mabao ya kufunga na kufungwa.