Mabingwa wa Europa League Manchester United, wameachana na mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji mahiri kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Atletico Madrid, Antoine Griezmann.
Uamuzi huo ambao umewashtua mashabiki wengi wa soka duniani, umetangazwa baada ya rufaa ya klabu ya Atletico Madrid ya kupinga kufungiwa kusajili wakati wa majira ya kiangazi, kuwekwa kapuni na mahakama ya usuluhishi ya michezo CAS.
Mapema mwaka huu Atletico Madrid na wapinzani wao Real Madrid walifungiwa kufanya usajili baada ya kukutwa na hatia ya kufanya udanganyifu kwenye usajili wa wachezaji wenye umri mdogo.
Manchester Utd imeamua kujiweka pembeni baada ya kugundua kuwa Atletico Madrid haitaweza kumuachia Griezmann kirahisi, licha ya hukumu hiyo ya FIFA kutoizuia klabu hiyo kuuza wachezaji.