Rais wa klabu ya FC Porto ya Ureno Jorge Nuno Pinto da Costa amesema mlinda mlango wa klabu hiyo Iker Casillas, yu mbioni kutangaza kustaafu soka, na huenda akajitosa kuwania nafasi ya urais wa shirikisho la soka nchini Hispania (RFEF).
Pinto da Costa alifichua siri hiyo jana jumanne alipozungujmza na waandishi wa habari mjini Porto kwa kusema, “Casillas amenieleza ukweli wa maamuzi ambayo anatarajia kuyachukua siku za hivi karibuni, atazungumza na nyinyi kwa undani zaidi, lakini ukweli ni kwamba amepanga kustaafu soka, na huenda akajitosa kuwania nafasi ya urais wa shirikisho la soka la nchini kwao Hispania.”
Casillas mwenye umri wa miaka 38, amekuwa katika wakati mgumu wa kutimiza majukumu yake uwanjani tangu mwezi Aprili mwaka jana, baada ya kupata shambulizi la moyo, jambo ambalo linahisiwa huenda limemsukuma kufikiria maamuzi ya kustaafu soka.
Mlinda mlango huyo alijiunga na FC Porto mwaka 2015 akitokea Real Madrid, na anaendelea kukumbukwa kwa mambo makubwa yaliyompa mafanikio katika soka ulimwenguni.
Casillas amewahi kutwaa ubingwa wa dunia akiwa na kikosi cha Hispania mwaka 2010, huku akicheza michezo 167 akiwa na timu hiyo, pia amewahi kutwaa ubingwa wa mataifa ya Ulaya mara mbili mfululizo (Euro 2008 na 2012).
Akiwa na Real Madrid alicheza michezo zaidi ya 700 na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Hispania (La Liga) mara tano, na ubingwa wa barani Ulaya (UEFA Champions League) mara tatu.
Kwa kipindi cha miezi kadhaa Casillas alikua anahusishwa na mpango wa kuwania nafasi ya urais wa shirikisho la soka nchini Hispania RFEF, kwa kumpa upinzani rais wa sasa Luis Rubiales.
Mwanzoni mwa juma hili Casillas alikaririwa akisema “Dhamira yangu ni kuwekeza nguvu katika shirikisho la soka nchini Hispania, ili kuendeleza mipango ya nchi yangu katika kucheza soka la ushindani na lenye kuvutia ulimwenguni “.
Rais wa sasa wa RFEF Rubiales, amekua na mgogoro dhidi ya rais wa La Liga Javier Tebas, katika mambo kadhaa hususan upande wa upangaji wa ratiba ya ligi ya nchini Hispania, jambo ambalo linatajwa kama kichocheo cha baadhi ya wajumbe kupanga kumuengua kupitia uchaguzi mkuu.
Uchaguzi wa rais wa RFEF umepangwa kufanyika baada ya michuano ya Olimpiki itakayounguruma Tokyo, Japan, baada ya Rubiales kuomba usogezwe mbele, ili kupisha fainali za mataifa ya Ulaya (Euro 2020), ambazo zitaanza kuunguruma Juni 12 hadi Julai 12.