Timu ya taifa ya Uruguay imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia, baada ya kuitoa timu ya taifa ya Ureno kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora.

Mabao ya Edinson Cavani katika dakika za 7 na 62 yametosha kuipeleka mbele timu hiyo ambayo mwaka 2010 iliinyima Ghana nafasi ya kucheza nusu fainali kwa tukio la Luis Suarez kudaka mpira uliokuwa unaelekea nyavuni. Bao la Ureno limefungwa na mlinzi Pepe dakika ya 55.

Baada ya Suarez kutoa msaada kwa bao la kwanza la Cavani, muunganiko wao sasa kati ya Luis Suarez na Edinson Cavani umetengeneza jumla ya mabao 4 kwenye Kombe la Dunia. Wanazidiwa na muunganiko wa Grezegorz Lato na Andrzej Szarmach wa Poland, mabao 5 na ule wa Michael Ballack na Miroslav Klose wa Ujerumani, mabao 5. Hii ni kuanzia mwaka 1966.

Kwa upande wake Cavani amefikisha mabao 3 kwenye fainali hizo hivyo kuwa nyuma ya Cristiano Ronaldo na Romelu Lukaku wenye mabao manne kila mmoja pamoja na Harry Kane mwenye mabao matano. Pia analingana na Kylian Mbappé, Diego Costa na Denis Cheryshev wenye mabao matatu kila mmoja.

Hata hivyo, hiyo pia imekuwa ni mara ya kwanza kwa Uruguay kushinda katika mechi tatu ambazo timu hizo zimecheza tangu mwaka 1972. Katika mechi mbili zilizopita Ureno ilikuwa imeshinda mara moja na kutoka sare mechi moja.

 

 

Video: Lissu atoboa siri ya dereva wake, Tajiri awatwanga risasi maofisa usalama taifa
Video: Dogo Janja aachia ngoma mpya 'Banana', itazame hapa