Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha mjini, Mkoani Pwani kimesema wakati chama kikielekea kwenye chaguzi mbalimbali ,wanaCCM wajipange kuchagua wagombea wanaokubalika na wananchi na wawajibikaji.

Aidha kimesema ushindi mkubwa uliopatikana katika uchaguzi mdogo uliopita uwe somo kuwa chaguzi bila rushwa inawezekana .

Mwenyekiti wa chama hicho mjini Kibaha, Maulid Bundala, amesema hayo katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM mjini hapo, kilicholenga kumpongeza Ramadhani Bogas kwa kushinda udiwani kata ya Misugusugu.

“Wakati tukielekea kwenye uchaguzi wa chama kuanzia ngazi ya chini, tunapaswa kuweka watu wanaokubalika katika jamii, wenye moyo wa kufanya kazi tubadilike wakati wa kubeba mizigo umepitwa ,tuchague wenye kukipenda na kuweza kukitumikia chama pasipo kununua uongozi “amesema Bundala.

Katibu wa CCM Mjini Kibaha, Abdallah Mdimu,amesema kuwa kama chaguzi zote zingekuwa zinafanyika hivyo basi CCM itaendelea kushika dola miaka mingi ijayo.

Amesema uchaguzi huo ulikuwa mwepesi kwani wagombea waliowekwa walikubalika na wananchi.

Mdimu amesisitiza umoja ,mshikamano  na kuondoa makundi ambayo wakati mwingine husababisha kuvuruga upatikanaji wa ushindi.

Katibu mwenezi wa CCM Mkoani Pwani, Zainab Gama, amempongeza Bogas kwa ushindi aliokipatia chama na kumuomba diwani huyo kusimamia ilani ya Chama cha Mapinduzi na kutembelea wananchi ili kujua kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake Bogas, alishukuru jumuiya zote na chama kijumla kupigana kwa umoja kupata ushindi huo, katika uchaguzi mdogo kata ya Misugusugu Ramadhani Bogas (CCM) alipata kura 1,307, Gasper Ndakidemi (Chadema) 926 na CUF 56.

Ombeni Sefue ateuliwa APRM
Wachimbaji 15 waokolewa wakiwa hai mkoani Geita