Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema amesema kuwa juzi Jumatano Februari 6, 2019 walilazimika kumuondoa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe baada ya kufuatiliwa na watu ambao hakuwataja.
Ameyasema hayo wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ambapo amesema kuwa kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitawala kwa haki, kwa kufuata sheria na Katiba hana tatizo hata kikitawala milele.
“Leo mwenyekiti (Mussa Azzan Zungu), Zitto hayuko bungeni tumemuondoa juzi alikuwa anafuatiliwa usiku kwa kazi za kibunge, sio za kuuza madawa ya kulevya si za kubaka watoto ni kazi za kibunge.”amesema Lema
Hata hivyo, Lema ameongeza kuwa lengo lao ni kuona wanatawaliwa kwa haki na ndio maana ya upinzani lakini leo hii chuki inajengwa na baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakitoa kauli tata dhidi ya upinzani.