Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitafanya uchaguzi wa mgombea urais kwa shinikizo na presha ya wa wapambe wa wagombea wanaowania nafasi hiyo.

Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, ametoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, siku moja kabla ya zoezi la mchujo wa wagombea 32 utakaofanywa na kamati kuu ya chama hicho kuwapata wagombea watano.

“CCM haitafanya uamuzi kutokana na msukumo wa wapambe wa wagombea, kwani kuna kanuni na taratibu na waliochukua fomu wanafahamu kuna kushinda na kushindwa, na asiyekubali kushindwa sio mshindani,” alisema Nape.

Alisema kuwa kanuni za chama hicho zinatoa muongozo wa namna ya kumpata mgombea kati ya waliotangaza nia na kurudisha fomu kwamba mchujo utafanywa kwa kuzingatia sifa 13 zilizoanishwa na chama hicho ambazo anapaswa kuwa nazo mgombea atakaepata points nyingi zaidi.

“Kanuni yetu inasema 5,3,1 kwani kutoka Kamati Kuu kwenda Halmashauri Kuu, tunachuja na kubaki na majina matano na uchujaji huo unafanyika na kikao hakitakiwi kutoa sababu,” alisema Nape na kuongeza kuwa mchujo wa pili utafanyika na watatoka kwenye wagombea watano na kubaki watatu na hatimaye atabaki mgombea mmoja atakaekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba, 2015.

Akiongea na BBC mapema leo asubuhi, Nape amesema kuwa aliamua kutoa kauli hiyo jana kwa kuwa wamegundua baadhi ya wagombea wamepeleka vijana wengi na wapambe mjini Dodoma kwa lengo la kutaka kushinikiza au kuweka presha ili mgombea wa kiti chao achaguliwe.

Nape amesikika pia kupitia TBC1 akieleza kuwa uchaguzi huo utakuwa wa haki kwa kufuata sifa 13 zilizotolewa na chama hicho na sio vinginevyo.

“Hata mwaka 1995, CCM ilipomchagua Benjamin Mkapa kuwania nafasi ya uras, watu walimfuata mwalimu Nyerere pale kwake Msasani wakamuuliza kwanini mmemchagua huyu. Aliwajibu kuwa ‘hata ungekuwa wewe ungemchagua huyu, kwa sababu ukiangalia sifa zilizoanishwa zinaonesha huyu amepata nyingi zaidi ya wenzake’,” alisema.
Julai 11, Mkutano Mkuu kupitisha Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 na kupigia kura majina matatu kupata jina moja.

Chadema Wakutana Kwa Dharura Kujadili Joto La Uchaguzi Mkuu
Vijana Wa Obama Wawaliza Wajapan Kombe la Dunia