Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kuwa kutunisha misuli au kuonesha ubabe sio sifa za mtu anaepaswa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali sifa za rais anaihitajika ni yule mwenye fikra safi na uwezo wa kufanya kazi kwa maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na kada wa CCM, Dk. Hamisi Kigwangalla aliyekuwa akiwakilisha chama chake kwenye mdahalo wa Mikikimikiki uliorushwa na kituo cha Star TV ambao uliwahusisha wawakilishi wa Ukawa, Chaumma na ACT-Wazalendo.

“Ni kweli kwamba Ikulu hapahitaji Tyson au mtu mwenye misuli, ikulu panahitaji mtu mwenye fikra safi na mwenye uwezo wa kufanya kazi,” alisema Dk. Kigwangalla.

“Lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba ikulu hatuhitaji mtu ambaye hana uwezo wa kuhutubia zaidi ya dakika 5. Lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba hatuhitaji kumpeleka ikulu mtu ambaye ataona wezi na wala rushwa wakiiba na akashindwa kuwakemea,” alisisitiza Dk. Kigwangalla na kuongeza kuwa Tanzania inahitaji mtu msafi na msomi wa sayansi kama alivyo mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.

“Hatuhitaji kuona mtu ambaye akiona wezi na wala rushwa wakiiba na akashindwa kuwakemea, tunahitaji ikulu aende mtu mwenye maarifa safi kama Dk. Magufuli, msomi wa sayansi na wala hatuhitaji mtu mwenye maarifa ya Sanaa na kufanya usanii, mwenye maarifa ya kufanya ulaghai,”alisema.

Hata hivyo, Dk. Kigwangalla alisema kuwa ikulu hapahitaji mtu goigoi bali mtu mchapakazi anayeweza kufanya kazi kwa muda mrefu na sio goigoi.

Awali muwakilishi wa Ukawa katika mdahalo huo, Dk. Onesmo Kyauke, aliibua hoja hiyo baada ya kutoa maelezo yaliyoungwa mkono na maelezo ya Dk. Kigwangalla kuhusu sifa za rais wa awamu ya tano anayehitajika kwa maendeleo ya Taifa.

Akionesha mlengo wa kumpigia debe mgombea urais wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa, Dk. Onesmo alieleza kuwa ili kuyatatua matatizo ya watanzania, ikulu inahitaji kuwa na kiongozi mwenye fikra pana aliyebeba maono ya taifa na kwamba kazi ya ikulu haihitaji mtu kuwa na misuli au mabavu ili atekeleze majukumu yake.

Kauli hizi zinakuja ikiwa ni siku chache baada ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli kuamua kupiga push up jukwaani alipokuwa akiwahutubia wananchi kwa lengo la kuwaonesha kuwa yuko ‘fiti’.

Magufuli: Sigombei Urais Kwa Majaribio, Nauweza
Lowassa Atangaza Mbinu Mpya Ya Kupambana Na Rushwa