Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo amesema CCM iko salama na imara katika kusimamia misingi, shabaha na malengo yake, ikiwemo kuendelea kuwa daraja la kusikiliza na kutatua changamoto za Wananchi.

Ndugu Chongolo ameyasema hayo alipokutana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid jijini Dar Es Salaam, kwa ajili ya kujitambulisha na kuanza kazi, baada ya kukabidhiwa ofisi zao rasmi na watangulizi wao.

Amesema, CCM inaendelea kuwatumikia wananchi kwa kuzisimamia Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar, ambazo zimeendelea kutafsiri maelekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, kwa vitendo.

Chongolo, aliwaelekeza Makonda na Hamid, kuanza majukumu yao, wakitambua imani kubwa waliyopewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Dokta Samia Suluhu Hassan, kutumikia Chama kupitia nafasi hizo walizoteuliwa.

Amesema kuwa nafasi hizo mbili, Idara ya Itikadi na Uenezi na Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati ya CCM, hivyo wanapaswa kujua kuteuliwa kwao ni sehemu ya kuongeza chachu na kasi ya idara hizo kutekeleza malengo yaliyokusudiwa na CCM, katika kutumikia wananchi na kuzisimamia Serikali zote mbili za CCM.

Ndugu Makonda na Ndugu Hamid, waliteuliwa kushika nafasi hizo, hivi karibuni na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), iliyoketi katika kikao chake maalum chini ya Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 22, 2023, jijini Dodoma.

Ibrahim Class, Majiha kupanda ulingoni
Mayele afunguka kuikataa Al Ahly, Mamelodi