Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba Jonathan Mkumba amesema Uwanja huo upo tayari kwa mchezo wa Nusu Fainali ya Kwanza Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ utakaopigwa Jumamosi (Mei 28).
Miamba hiyo ya Soka la Bongo Simba SC na Young Africans imepangwa kucheza Uwanja hapo, baada ya kuvuka hatua ya Robo Fainali ya ‘ASFC’, iliyofikia tamati Jumapili (Mei 14).
Mkumba amesema Maboresho katika eneo la kuchezea yamekamilika na nyasi zipo katika ubora, hivyo kinachoendelea kwa sasa ni maboresho madogo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na chumba cha matibabu upande wa Mashabiki.
Amesema Uwanja huo umekua kwenye marekebisho makubwa tangu mwezi Machi mwaka huu, baada ya kupata maagizo kutoka TFF ambayo yaliainisha sehemu za kufanyiwa Ukarabati/Maboresho ili kukidhi hadhi ya kuhodhi mchezo wa Nusu Fainali.
“Tulipokea maagizo kutoka TFF, kwa asilimia kubwa tumekamilisha kila hatua tulioagizwa kuifanyia ukarabati, tulikwangua nyasi za zamani na tukapandikiza nyasi mpya, na kwa sasa zipo tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki hapa Mwanza na kwingineko.”
“Kwenye vyumba vya kubadilishia nguo tumeboresha kwa kupaka rangi upya, tumerekebisha miundombinu ya vyoo na maji iliyokua imeharibia, mafundi wapo katika hatua za mwisho kuweka masinki ya vyoo.”
“Vyumba vya waamuzi pia tumefanya marekebisho kwa kupaka rangi upya, pamoja na kutengeneza vitu vidogo vidogo vilivyokua vinahitaji kufanyiwa marekebisho” amesema Jonathan Mkumba
Simba SC ilitinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho kwa kuichapa Pamba FC ya Mwanza mabao 4-0, huku Young Africans ikiifurusha Geita Gold FC kwa changamoto ya Penati baada ya timu hizo kufungana 1-1 ndani ya dakika 90.