Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe wameeleza siri ya mafanikio yaliyofikiwa na chama hicho miaka michache tangu mkoa huo ulipoanzishwa.
Akizungumza mbele ya viongozi wa CCM mkoa wa Njombe mlezi wa chama hicho mkoani humo, Dkt. Frenk Hawasi ameupongeza uongozi wa chama hicho kwa kufanikisha ujenzi wa Ofisi kubwa ya chama katika eneo la Mjimwema mjini Njombe ndani ya muda mfupi tangu mkoa huo uanzishwe.
‘’Ndg,zangu nawapongeza sana nadhani nilifika hapa mwaka jana hali haikuwa hivi naona mnajengo la kiutu uzima hapa ninavyo wafahamu ndugu zangu wa Njombe ni wachapa kazi naamini mliamua kushirikiana na wanachama hadi mmefanikiwa, ipo baadhi ya mikoa ilianzishwa zamani kuliko Njombe lakini haina Ofisi kama hii hongereni sana,’’amesema Dkt. Hawasi
Aidha, kwa upande wake katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoa wa Njombe, Erasto Ngole amesema kuwa siri kubwa ya mafanikio hayo ni umoja na mshikamano uliopo kati ya viongozi na wanachama wa CCM kutoka wilaya zote za mkoa wa Njombe walioamua kutoa michango yao hadi kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo kubwa na ya kisasa.
Hata hivyo, Ngole ameongeza kuwa jengo hilo limejengwa kwa usimamizi mkubwa wa aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe, Deo Sanga(Jah People) ambaye kwasasa ni mbunge wa jimbo la Makambako pamoja na aliyekuwa katibu wa CCM mkoa wa Njombe Ndg. Hosea Mpagike ambaye kwasasa amestaafu baada ya kukitumikia chama kwa muda mrefu.