Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe, Erasto Ngole amesema kuwa chama hicho kitaibuka na ushindi mnono katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Makambako waliojitokeza kumsikiliza Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson, ambapo amesema kuwa chama kimeendelea kuisimamia Serikali ili itekeleze ahadi zake kwa wananchi mkoani Njombe.
‘’Mh. Naibu spika nakuhakikishia kuwa katika uchaguzi huu wa Serikali za mitaa ushindi kwa chama cha mapinduzi ni lazima kutokana na jinsi chama kinavyo isimamia serikali inayoongozwa na chama hiki na wananchi wa mkoa wa Njombe wanaona jinsi sisi viongozi wa chama tunavyo shughulika na shida zao,’’amesema Ngole.
Aidha, amesema kuwa Serikali imeboresha miundombinu katika vijiji vya mkoa wa Njombe ikiwemo kupeleka miradi ya maji, Barabara, mawasiliano ya simu pamoja na kujenga Zahanati na vituo vya Afya ambavyo baadhi ya hivyo Rais Magufuli ametoa pesa za kutosha kukarabati na kupanua vituo hivyo.
Baadhi ya wabunge walioshiriki ziara hiyo ni pamoja na mbunge wa Jimbo la Makambako mh.Deo Sanga, mbunge wa jimbo la Lupembe mh.Joramu Hongoli pamoja na wabunge wa viti maalumu wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe Dkt. Susan Kolimba na Neema Mgaya kwa pamoja wameahidi kushirikiana na wananchi ili chama kishinde katika uchaguzi huo wa Serikali za mitaa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Njombe na kaimu mkuu wa mkoa huo, Ruth Msafiri amesema kuwa hali ya mkoa wa Njombe imeendelea kuimarika kiusalama kila siku huku akiwataka wananchi mkoani humo kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali kwa uhuru na amani bila hofu yeyote.