Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kimewaomba radhi wafanyabiashara wa halmashauri ya mji wa Makambako kutokana na usumbufu uliojitokeza dhidi yao na serikali wakati wa kutatua tatizo la mauaji ya watoto mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho mkoa wa Njombe, Erasto Ngole ambapo amesema chama hicho kimeona umuhimu wa kuomba radhi kutokana na kuwahusisha wafanyabiashara wa mji huo katika matukio ya mauaji huku wengi wakisumbuliwa kuhojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Katibu huyo amewatoa hofu wafanyabiashara wa Mji wa Makambako ambao walikuwa na imani kuwa viongozi wa chama hicho pamoja na Serikali mkoani Njombe walikuwa wakiwahusisha na mauaji hayo ya watoto.
‘’Waandishi wa habari mimi ndiye msemaji wa chama cha mapinduzi naomba niseme kuwa pale Mji wa Makambako wakati wa kutafuta namna ya kuzuia mauaji ya watoto baadhi ya wafanyabiashara pale walikuwa wakituhumiwa lakini wakati tukikemea wengine walisema tunawakera, kwa niaba ya chama na Serikali tunaomba watusamehe kwasababu ile ilikuwa ni sehemu ya kutafuta amani,’’ amesema Ngole.
Aidha, amesema kuwa wananchi mkoani humo wanapaswa kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali kama kawaida bila hofu yeyote kwakuwa hali ya usalama katika mkoa huo kwasasa imeimarika kutokana na jeshi la polisi kwa kushirikiana na serikali kumaliza tatizo hilo.
Hata hivyo, siku chache zilizopita mkoa wa Njombe uligubikwa na tatizo la mauaji ya watoto lakini kwa sasa tatizo hilo limekwisha na tayari watuhumiwa saba waliohusika na mauaji wameshafikishwa mahakamani kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa kwaajili ya hatua zaidi za kisheria.