Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Njombe kimewataka wananchi mkoani humo kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali kama kawaida bila hofu yeyote kwakuwa hali ya usalama katika mkoa huo kwasasa imeimarika hakuna tatizo lolote.

Hayo yamesemwa mkoani humo na Katibu wa siasa na uenezi wa chama hicho, Erasto Ngole ambapo amesema kuwa Uongozi wa Chama hicho umepokea taarifa ya kuimarika kwa usalama kutoka kwa viongozi wa ulinzi na usalama wa mkoa huo.

Amesema kuwa siku chache zilizopita mkoa wa Njombe ulikumbwa na tatizo la mauaji ya watoto lakini kwasasa tatizo hilo limekwisha kutokana na vyombo vya ulinzi na usalama kuwadhibiti wahusika wa matukio hayo ambao tayari wameshaanza kufikishwa mahakamani kwaajili ya hatua zaidi za kisheria.

‘’Baadhi ya wananchi bado hawaamini kama usalama umeimarika tunawomba waandishi wa habari mtusaidie kuwaelekeza wananchi kuwa sasa hali ni shwari na wauaji saba tayari wapo magereza na vifo nane vilijitokeza katika matukio haya,’’ amesema Ngole

Aidha, katibu huyo wa siasa na uenezi wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kwa niaba ya chama amewatoa hofu wafanya biashara wa Mji wa Makambako ambao walikuwa na imani kuwa viongozi wa chama hicho pamoja na Serikali mkoani Njombe walikuwa wakiwahusisha na mauaji hayo ya watoto akisema kuwa hali hiyo ya malumbano ili jitokeza kutokana na kutafuta amani ili mkoa wa Njombe ubaki salama.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kimetoa maagizo kwa viongozi wa chama hicho mkoani humo kuacha tabia ya kukaa ofisini badala yake watoke na kushuka kwa wananchi vijijini.

 

Majaliwa awaonya wafanyabiashara kuhusu rushwa
Video: Ukaguzi wa maduka ya fedha watikisa Dar, Maelfu ya Walimu kuajiriwa nchini