Kuelekea maandalizi ya chaguzi za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwakani na uchaguzi Mkuu mwaka 2025, Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa wa Pwani wamepewa semina elekezi kwa lengo la kuwajengea uwezo, kwa ajili ya kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Pwani, David Mramba mjini Bagamoyo wakati akizungumzia semina elekezi hiyo ya siku tatu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Taifa Comred Sofia Mjema kwa Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya name za mkoa huo.
Amesema, lengo la Semina hiyo ni kujenga uwezo wa kuhamasisha Watanzania kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kuhakikisha Taifa linapiga hatua za maendeleo.
“Yapo maelekezo sisi Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wa mikoa hapa nchini kutoka kwa Katibu wa NEC Comred Sofia Mjema kwaajili ya kuwashushia Makatibu wa Siasa na uenezi wa ngazi ya wilaya mafunzo haya yataenda kuwa chachu ya hamasa katika maeneo yetu ya Mkoa wa Pwani” amesema Mramba.
Aidha, mewataka Makatibu hao wa Siasa na Uenezi wa CCM kutoka Wilaya za mkoa wa Pwani kuwa ni Ramadhani lukanga (Bagamoyo), Clemence Kagaruki (Kibaha mjini), Juakali Kuwanya (Kibiti), Hamisi biggo (Kibaha Vijijini), Issa Mtulyakwaku (Rufiji), Issa kombo (Mafia), Haruna meza (Kisarawe) na Kisatu o. Kisatu (Mkuranga).
Ameongeza kuwa, Idara ya uenezi ni idara kamili ndani ya CCM idara hii ndio inayoweza kukifanya Chama hiki kisonge mbele na ndio idara hii inayoweza kukifanya Chama chetu kirudi nyuma, kitasonga mbele kwa kutangaza kazi zilizofanyika serikalini kupitia Chama cha mapinduzi.
“Lakini Idara ya uenezi isipotangaza kazi hizo maana yake tutakuwa tunajirudisha nyuma niwaombe ndugu zangu kasimamieni majukumu na kazi zetu katika wilaya zenu kwa uaminifu mkubwa” amesema Mramba.
Semina hiyo elekezi imezingatia katiba ya CCM Ibara ya 98 lakini pia kwenye toleo jipya la mwaka 2021 linazungumza kuhusu majukumu ya Katibu wa Siasa na Uenezi ngazi ya mkoa na inaelekeza majukumu hayo kwenye ngazi ya Wilaya na Kata, shina na matawi.
“Kuelekea chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji mwakani na uchaguzi Mkuu mwaka 2025 Ninaamini kabisa kwa mafunzo haya wamepata uelewa wa kufanya kazi yao vizuri hususani katika kuingiza wanachama kwa wingi, kuwafanya wanachama walio ndani ya CCM kutokutoka nje kwenda kwenye vyama vya upinzani” amesema Mramba.