Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya kimekamata kadi bandia za chama hicho ambazo zinadaiwa kutumika kufanya hujuma katika mchakato wa uchaguzi.

Kadi hizo bandia zinaaminika kuwa zilitumika katika mchakato wa kura za maoni za kuwachagua wagombea wa nafasi ya urais, ubunge na madiwani zilizofanyika hivi  karibuni na kugubikwa na vurugu na malalamiko.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Mbeya, Bashir Madodi amesema kuwa wamebaini uwepo wa kadi nyingi bandia katika mkoa huo baada ya kuwepo ongezeko la kadi mpya amabazo hazikutoka katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam.

“Kwa kawaida kadi zinatoka makao makuu, zikifika hapa mkoani zinasajiliwa. Namba zikishasajiliwa ndipo zinapelekwa wilayani. Sasa kuna kadi nyingi ambazo zinaonekana ambazo hazikusajiliwa katika mkoa wetu. Kwa hiyo zile kadi sio halali kwa mkoa wetu. Na ndizo zimeonekana kutaka kupiga kura za maoni katika vituo vyetu vya kupigia kura,” alisema Madodi.

Hata hivyo, hofu ya chama hicho juu ya kadi hizo bandia inahamishiwa kwenye vyama vya upinzani. Chama hicho tawala kinaamini kuwa kadi hizo bandia ndizo ambazo hutumiwa na vyama vya upinzani kutengeneza propaganda ya kisiasa na kuonesha kuwa wana CCM wamerudisha kadi nyingi.

“Tumekuwa tunajaribu kufanya utafiti wa muda mrefu, kwamba ‘kwanini kadi zinaporudishwa mara kwa mara kwenda upinzani zinakuwa ni kadi mpya na sio kadi za zamani’? ndio tumekuja kubaini kuwa ni pamoja na hilo,” Madodi aliviambia vyombo vya habari.

Uchaguzi wa kura za maoni za CCM katika sehemu mbalimbali zimegubikwa na migogoro mikubwa hali iliyopelekea wagombea wengi kukata rufaa kupinga matokeo hayo katika ngazi za juu za chama hicho. Sehemu nyingi, hesabu ya kura zilizopigwa inaonesha kuwa kubwa kuliko idadi halisi ya wapiga kura huku maeneo mengi yakiwa bado yanavutana kutangaza matokeo kutokana na hujuma mbalimbali.

Shaqiri Kukamilisha Usajili Stoke City
Seydou Doumbia Arejea Nchini Urusi