Boniface Gideon – TANGA.
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi – CCM, Mkoa wa Tanga ikiongozwa na Mwenyekiti wake Rajab Abdurhamani imeonesha kukerwa na kitendo cha baadhi ya miradi kusuasua, huku baadhi ikikumbwa wizi wa vifaa ikiwemo katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani.
Hayo yalibainika leo wakati wa ziara ya kamati ya siasa yakukagua miradi wilayani hapa iliyokuwa na lengo la kufuatilia maagizo yake yaliyotolewa wakati wa ziara yake ya hivi karibuni ambapo Kamati hiyo, pia imetoa maagizo kwa Vyombo vya Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na watakaowabaini walihusika kwenye tukio hilo hatua kali za kisheria zichukuliwe.
Mwenyekiti wa CCM, Tanga Abdulrahman alisema pamoja na hayo wachukuliwe hatua za kinidhamu na asionewe mtu huku akisisitiza aliyetia mkono wake kuiba vifaa hivyo ashughulikiwe na akiwa Hospitalini hapo baada ya kukagua ukarabati wa Hospitali hiyo unaogharimu milioni 900, Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah alielezea wizi huo.
Mwenyekiti huyo alisema, “tutawapa lawama ndugu zetu waliopewa nafasi ya kusimamia miradi ikiwemo Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya na katika hili nikutake Mkuu wa wilaya usicheke na mtu na ukiacha hilo ninazo taarifa nyingine nitakapo zithibitisha nitachukua hatua kuna vifaa viliibwa hapa hospitali lakini jana usiku baada ya kusikia ninakuja vimerudishwa watu hawaogopi wala hawana haya hilo halikubaliki.”