Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitashiriki kwenye mdahalo uliotarajiwa kuwahusisha wagombea urais wote, ikiwa mgombea wa Chadema, Edward Lowassa hatakuwa miongoni mwa wagombea urais wa vyama vya upinzani watakaoshiriki.

Hayo yamesemwa jana na mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba jijini Dar es Salaam alipokuwa anazungumzia uamuzi wa chama hicho kufuatia mualiko wa kushiriki mdahalo wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopangwa kufanyika Jumapili, Oktoba 13.

“Tumeeleza mara nyingi utayari wetu wa kushiriki mdahalo, lakini tutashiriki tu endapo mgombea wa Chadema atashiriki pia,” January Makamba anakaririwa na gazeti la Citizen.

Alieleza kuwa mdahalo huo hautakuwa na maana endapo hautawahusisha wagombea wawili wenye nguvu zaidi ambao ni wa chama chake, Dkt. John Magufuli pamoja Edward Lowassa wa Chadema.

Hii ina maanisha kuwa watanzania hawatawashuhudia wagombea urais wa CCM na Chadema katika mdahalo huo, kwa kuwa Chadema wamesisitiza kuwa hawataweza kumpeleka mgombea wao kutokana na ratiba ya kumalizia kampeni.

“Itatugharimu sana kumtoa mgombea wetu kwenye ratiba ya kampeni kumleta Dar es Salaam na kumrudisha tena kwenye kampeni. Lakini pia muda kampeni umebaki mfupi sana kwetu,” Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene.

Kwa mujibu wa waandaaji wa mdahalo huo, hadi kufikia jana (Oktoba 12), ni vyama vitatu pekee vilivyokuwa vimethibitisha ushiriki wao. Vyama hivyo ni ADC, ACT-Wazalendo na CHAUMMA.

Mdahalo huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa mashirika ya CEO Round Table, Twaweza na Tanzania Women’s Media.

Endapo Dkt. Magufuli angeshiriki katika mdahalo huo, angekuwa mgombea wa kwanza wa urais kupitia CCM kushiriki katika mdahalo wa wagombea urais tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Mzee Kingunge, Ya Ukweli Haya Kuhusu Lowassa na CCM!?
Magufuli Asema Wagombea Wa Upinzani Ni Chanzo Cha Mgao Wa Umeme