Kampeni za uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar zimeanza kwa kasi huku vyama viwili vyenye nguvu zaidi, CCM na CUF vikivutana mashati katika kuwashawishi wapiga kura.

CCM imeanza kwa kasi kumshambulia mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni makamu wa kwanza wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar. Kwa nyakati tofauti, viongozi wa chama hicho wamemuelezea Maalim Seif kama mnafiki na muongo kufuatia ahadi nono za kuwaletea wananchi maendeleo makubwa.

Mwenyekiti wa CCM taifa, Dk Jakaya Kikwete alimuelezea Maalim Seif kama mnafiki anaedai serikali iliyokuwa inaongozwa na Dk. Ali Shein haikuwaletea wananchi maendeleo wakati yeye na viongozi wengine wa CUF walikuwa sehemu ya serikali hiyo.

Alisema kama Maalim Seif aliona serikali hiyo ilikuwa inakosea katika utendaji wake na yeye akiwa sehemu yake angechukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi yake.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alida kuwa Maalim anawadanganya wananchi kwa ahadi yake ya kuigeuza Zanzibar kuwa kama Singapole.

“Nimemsikia Maalim anasema akiwa rais ataigeuza Zanzibar kuwa kama Singapole, wakati na yeye alikuwa sehemu ya serikali hii. Basi angetuonesha hata angalau nusu ya Singapole,” alisema jana Kinana huku akiwasihi wananchi wa Zanzibar kutomsikiliza mgombea huyo wa CUF anayeungwa mkono na Ukawa.

Kadhalika, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wake, Shaka Hamdu Shaka, ulimtaka Maalim Seif kuacha kuupotosha umma kwa kudai kuwa CCM haijawaletea wazanzibar maendeleo.

Umoja huo pia ulikosoa ahadi ya Maalim Seif ya kutoa ajira kwa vijana wote wa Zanzibar endapo atakuwa rais wa Zanzibar. UVCCM walieleza kuwa mgombea huyo anawadanganya wananchi wa Zanzibar kwa kuwa alishindwa kuonesha mfano huo alipokuwa sehemu ya serikali.

UVCCM walieleza kuwa serikali hiyo imetekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwaletea maendeleo wananchi yakiwemo kukuza uchumi, kuboresha miundombinu,utalii, kuboresha elimu pamoja na huduma za afya.

CCM jana ilizindua rasmi kampeni zake visiwani Zanzibar katika viwanja vya Kibanda Maiti.

Wagombea 14 wa urais wamepitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar kugombea urais kupitia vyama vyao vya siasa.

 

Diamond Amshawishi Nay Wa Mitego Kuhamia CCM , Nay Amkazia
Kwanini Ukawa Hawazumgumzii Ufisadi? Tundu Lissu aeleza