Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Serikali kumfungulia mashtaka ya uchochezi waziri mkuu wa zamani ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema kuwa kauli ya Lowassa kuhusu viongozi wa Uamsho ni ya kichochezi na hatari kwa amani ya nchi, hivyo hapaswi kuvumiliwa.
Polepole aliongeza kuwa haikuwa mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo mkongwe kutoa kauli za aina hiyo kwani aliwahi kutoa kauli za kibaguzi akiwa kanisani wakati wa kampeni za urais mwaka 2015.
“Haikuwa mara ya kwanza kutoa maneno ya kibaguzi na ya kichochezi. Alifanya hivyo wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 alipodai kuwa ni wakati wa kanisa fulani kushika nafasi ya urais. Tunalaani kwa nguvu zote kauli hizo,” Polepole anakaririwa.
Hata hivyo, Lowassa ambaye jana alifika kwa mara ya pili Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuhojiwa, alisema kuwa hatabadili msimamo wake kwa kile alichokisema wakati wa kushiriki futari iliyoandaliwa na madiwani wa Chadema jijini Dar es Salaam kuhusu viongozi hao wa Uamsho.
“Nasimamia nilichozungumza kwa sababu naamini katika demokrasia. Ninaamini niko sahihi. Watu hawa waondolewe magerezani, na mwenye mamlaka ya kuwatoa mbali na mahakama ni Rais,” alisema Lowassa.
Juni 27, mwaka huu Lowassa aliitwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano. Aliitikia wito na kuhojiwa kwa takribani saa nne. DCI alimtaka mwanasiasa huyo kurejea ofisini hapo jana ambapo alifika na kupangiwa kuripoti tena katika ofisi hiyo Julai 13 mwaka huu.