Chama Cha Mapinduzi mkoani Arusha kimepata pigo baada ya mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Onesmo Ole Nangole na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Mkoa, Isack Joseph maarufu kama ‘Kadogoo’ kukihama chama hicho na kumfuata Edward Lowassa katika Chama Cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA).

Ole Nangole na Isack Joseph walitangaza uamuzi wao huo jana mbele ya waandishi wa habari wakidai kutoridhishwa na muenendo wa chama hicho kwa ujumla hususan wakati wa mchakato wa kura za maoni na upitishaji wa jina la mgombea wa nafasi ya urais uliofanyika mjini Dodoma.

Akizungumza kwa msisitizo, Ole Nangole alisema kuwa amelazimika kuchukua uamuzi huo ingawa amekitumikia chama hicho kama mwanachama na kiongozi katika ngazi za wilaya na mkoa tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 1977 kwani ameona kuwa kimeacha misingi kilichoridhi kutoka TANU na misingi iliyowekwa na waasisi wa chama hicho.

“Miaka yote tangu nilipojiunga na CCM mwaka 1977, sikuwahi kuona kukiona chama hiki kikiendesha mambo yake bila kufuata kanuni na taratibu za vikao kama kilivyofanya wakati wa kupitisha jina la mgombea urais mjini Dodoma hivi karibuni,” alisema Ole Nangole.

“Kuondoka kwangu kumechangiwa na kikundi cha viongozi wachache kuiongoza CCM kwa mabavu, nguvu na kwa kutumia fedha walizokwapua serikalini,” Mwenyekiti huyo alisema na kuongeza kuwa chama hicho hakikumtendea haki Edward Lowassa na kumnyanyasa kwa kuzingatia kuwa ni kada aliyekitumikia kwa muda mrefu na kushika nyadhifa mbalimbali.

Kwa upande wa aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa mkoa huo, Issack Joseph, alimtaka Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuchunga kauli zake na kuacha kuwaita ‘Makapi’ watu wanaokihama chama hicho.

“Watasema mengi na tumeondoka watatuita makapi. Naomba nimwambie sisi sio makapi. Wakitaka tuzungumzie suala la makapi, hao nidio makapi halisi. Sisi watanzania sio makapi, kwa sababu tukichambuana kwa suala la makapi na kuangalia wewe umekwenda wapi tutakwenda kusiko,” alisema Joseph.

 

 

Tume Ya Taifa Kuchunguza Taarifa Za Ukusanyaji Vitambulisho Vya BVR Vya Askari
Babu Wenger Akataa Kumlaumu Cech