Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa karipio lingine kwa makada wake walioanza kufanya kampeni na kuunda makundi kwa lengo la kupata nafasi ya kugombea urais wa Zanzibar 2020.
Karipio hilo limetolewa na kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika wiki hii jijini Dar es Salaam; na kutangazwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.
“Kwa kuanza kufanya kampeni za kificho na za wazi kwa Urais wa Zanzibar ni kwenda kinyume na utamaduni na desturi njema za chama chetu ambazo kwa pamoja hutuongoza kuwapata viongozi wa CCM na Serikali zake,” Polepole anakaririwa.
Kwa upande mwingine, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM upande wa Zanzibar, Catherine Nao alisema kuwa kutokana na kauli hiyo kutolewa na viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho, inamaanisha kuwa wanaosaka urais kwa kampeni za chinichini wapo ndani ya Serikali au hata nje ya Serikali.
Alisema kuwa watu wanaofanya hivyo wanapaswa kuacha mara moja vinginevyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hicho.
Dkt. Ali Mohammed Shein anatarajia kufikia ukomo wa muda wake wa urais mwaka 2020 kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.
Kauli za onyo kwa wanaofanya kampeni za chinichini ziliwahi kutolewa na Rais Shein na Katibu MKuu wa chama hicho, Bashiru Ally kwa nyakati tofauti.