Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeteua majina matatu ya wagombea wa nafasi tatu za Ubunge katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 13 mwakani, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole amewataja Monko Justine Joseph (Singida Kaskazini), Damas Ndumbaro (Songea Mjini) na Dkt Stephen Lemomob Kiruswa (Longido).
Moja kati ya majimbo ambayo yanavuta usikivu wa watu wengi ni jimbo la Singida Kaskazini ambalo liliachwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake, Lazaro Nyalandu ambalo tayari CCM imeweka karata yake. Nyalandu alihamia Chadema.
Hata hivyo, Chadema imeitaka NEC kuahirisha tarehe ya uchaguzi na kuitisha mkutano na vyama vya siasa kuzungumzia yaliyojili katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliopita na kwamba wanaweza kususia uchaguzi mdogo wa wabunge.
NEC imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa haitabadili tarehe ya uchaguzi iliyotangazwa.