Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetangaza kuwa michuano ya CECAFA Kagame Cup 2023 haitafanyika.
Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA Auka Gecheo amesema kuwa mashindano hayo yaliyokuwa yakitarajiwa Kufanyika yamefutwa kwa sababu ya Kutokuwa na muda wa Kutosha Kutokana na kalenda za Mashindano ya CAF/FIFA
“Ni bahati mbaya kwamba kwa mara nyingine tena hatutakuwa na mashindano haya mwaka huu. Tulikuwa na matumaini ya kuandaa michuano hiyo ili kusaidia pia timu zetu za ukanda huu kutumia kujiandaa na mashindano ya CAF yatakayoanza mwezi ujao,” ameongeza Gecheo.
Ikumbukwe kuwa Michuano ya mwisho ya Kombe la Kagame ya CECAFA ilifanyika 2021 wakati Express FC ya Uganda ilipoifunga wageni Nyasa Big Bullets FC kutoka Malawi 1-0 katika fainali iliyochezwa Dar es Salaam, Tanzania.
Gecheo pia ameweka wazi kuwa michuano ya CECAFA U-23 iliyokuwa ikipangwa kufanyika nchini Ethiopia sasa itachezwa mwaka ujao mwezi Januari.
Pia Mashindano ya CECAFA U-18 kwa upande wa Wanawake yatafanyikaTanzania Julai 25 huku michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya CAF kwa Kanda ya CECAFA itafanyika nchini Uganda Agosti 12-30, wakati michuano ya CECAFA kwa Vijana U-15 itafanyika Novemba 4-18 nchini Uganda.
Kenya itakuwa mwenyeji wa Michuano ya CECAFA ya Wavulana U-18 kati ya Novemba 25 na Desemba 9, na kufuzu kwa Kanda kwa Mashindano ya Shule za Pan African baadaye Desemba.