Baraza la Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limetangaza michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 itakayoanza kutimua vumbi lake Novemba 22 jijini Arusha.

Rais wa CECAFA ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia, amezungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam maapema hii leo na kusema, michuano itashirikisha nchi tisa huku nchi mbili zikishindwa kuthibitisha ushiriki wao.

Karia amesema michuano hiyo ilikuwa ifanyike mwezi Aprili mwaka huu nchini Sudan, lakini kutokana na kuibuka na homa ya mafua ya Corona (COVID 19), ikabidi kuahirishwa na ndio yatafanyika mwishoni mwa juma hili.

Karia ameongeza michuano hiyo itakuwa na vituo viwili vya Arusha na Karatu huku timu zikigawanywa kwenye makundi matatu.

“Kundi B na C michezo yake itachezwa Arusha mjini na michezo ya kundi A ambapo Tanzania ndipo ilipo michezo yake itachezwa Karatu.” Amesema Karia.

Wakati huo huo katibu mkuu wa TFF Wilfred Kidao akazungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari kwa kueleza maandalizi kwa ujumla kuelekea kwenye michuano hiyo ambayo rasmi itaanza Novemba 22 mkoani Arusha.

“Maandalizi yote kwa ujumla yameshakamilika, sisi kama wenyeji tumefurahi michuano hii kuletwa hapa Tanzania, kwa mara ya kwanza tutautumia uwanja wa kisasa uliopo Karatu, huu uwanja una sehemu nzuri na bora ya kuchezea.” Amesema Kidao.

Timu zitakazoshiriki ni wenyeji Tanzania Bara, Zanzibar, Somalia, Djibouti, Kenya, Uganda, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini huku Eritrea na Rwanda ndio pekee ambao hawata shiriki.

Washindi wawili wa michuano hiyo watauwakilisha ukanda wa CECAFA kwenye fainali za Afrika chini ya umri wa miaka 20, zitakazofanyika mwakani katika visiwa vya Mauritania.

Mkurugenzi Jamii Forums ahukumiwa
Deeney: Lukaku alistahili kubaki Old Trafford