Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Young Africans kutoka nchini Burundi, Cedric Kaze huenda asiwe katika sehemu ya Benchi la Ufundi la timu hiyo, kutokana na kushindwa kufikia muafaka na mabosi wake katika mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.
Kaze ni sehemu ya viongozi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo, ambalo limeipa mafanikio makubwa Young Africans katika msimu uliopita huku wakimaliza mikataba yao ya kuendelea kubakia hapo.
Tayari aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia Nasreddine Nabi ameondoka klabuni hapo huku akitajwa kujiunga na klabu ya FAR Rabat ya nchini Morocco.
Inaelezwa kuwa Kaze ameshindwa kufikia muafaka mzuri wa kuongeza mkataba mpya wa kubakia hapo kutokana na Young Africans kushindwa kufika katika mshahara ambao anataka alipwe.
Mtoa taarifa hizi amesema kuwa, uongozi umeweka mshahara mdogo ambao yeye ameukataa huku akiomba aboreshewe zaidi ya ule ambao aliokuwa akilipwa awali ni siri.
Ameongeza kuwa rasmi mazungumzo yamefungwa kwa pande zote hizo mbili, na hivi sasa ameachiwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, Muargentina, Miguel Gamondi kutafuta kocha msaidizi atakayekuja kufanya naye kazi.
“Uongozi wa Young Africans wamemtega Gamondi wakimuachia nafasi ya kutafuta wasaidizi wake watatu katika benchi lake la ufundi wakiwemo kocha wa mazoezi ya viungo, kocha wa makipa na mtaalamu wa kuchambua mikanda ya wapinzani.
“Nafasi hizo ziliachwa wazi kufuatia kuondoka kwa Milton Nienov ambaye alikuwa kocha wa makipa, Helmy Gueldich aliyekuwa kocha wa mazoezi ya viungo na Khalil Ben Youssef na Kaze ambao wote mikataba yao imemalizika.
“Yalikuwepo mazungumzo yanaendelea kati ya Kaze na uongozi wa Young Africans ambayo yameshindwa kufikia muafaka mzuri baada ya yeye kutaka aboreshewe mshahara wake, upo uwezekano mkubwa wa kocha huyo kutoendelea hapo,” amesema mtoa taarifa hizi.
Afisa Habari wa timu hiyo, Ally Kamwe hivi karibuni alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Suala la Kaze lipo chini ya kocha wetu mpya Gamondi ambaye yeye ndiye atakayeamua, kwani kama akipendekeza alete benchi jipya basi tutaangalia nafasi nyingine tutakayompa katika timu.”