Kocha Msaidizi wa Young Africans Cedrick Kaze amesema hakuna anayependezwa na matokeo walioyapata kwenye michezo mitatu iliopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Young Africans imeambulia matokeo ya bila kufungana dhidi ya Simba SC, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons, hali ambayo imesababisha majonzi kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo.
Kocha Kaze amesema sio kwa Mashabiki na Wanachama wanaopitia hali hiyo pekee yao, bali hata Wachezaji na Benchi la Ufundi linahuzunika na kilichotokea kwenye michezo hiyo mitatu.
Hata hivyo Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema bado wanaendelea kusaka dawa ya kumaliza tatizo linalowakabili kwa sasa, huku akiwataka Mashabiki na Wanachama kuendelea kuwa na imani na timu yao.
“Matokeo mabaya ni kweli yanaumiza hata sisi makocha hakuna anayefurahia kuona timu yake haipati matokeo mazuri, tunaumia sana lakini hatuna jinsi, cha msingi tunaangalia mechi zijazo tufanye vizuri.”
“Najua wanaumia sana kuona timu haifanyi vizuri lakini wajue Mungu huenda kuna kitu kikubwa ametuandalia huko mbele, habari za kulalamika hadi kupitiliza sio vizuri zinatuvunja moyo wachezaji.” amesema Kaze
Licha ya kuambulia matokeo ya sare kwenye michezo mitatu mfululizo, Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 57, ikifuatiwa na Bingwa Mtetezi Simba SC yenye alama 46.