Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Cedric Kaze, yupo njiani kutangazwa kuwa sehemu ya Benchi la Ufundi la Namungo FC.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Kaze yuko kwenye mazungumzo na uongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi ambalo kwa sasa liko chini ya kocha Denis Kitambi.
“Kaze anakuja kuwa kocha mkuu na Kitambi atakuwa msaidizi huku Nsajigwa (Shadrack) akiendelea na majukumu yake ya kocha wa viungo,” kilieleza chanzo makini ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo, alipotafutwa Katibu Mkuu wa Namungo FC, Ally Suleimani, ili kujua ukweli wa taarifa hizo, ambaye alisema watafanya maboresho kwa kuongeza nguvu katika benchi lao la ufundi na suala hilo linafanyiwa kazi na kamati ya mashindano kulingana na mahitaji ya timu hiyo.
“Timu yetu ipo Karatu chini ya kocha wetu Kitambi akisaidiana na Nsajigwa, ninaimani kutakuwa na maboresho ambayo yanafanywa na kamati husika,”amesema Katibu huyo.
Kuhusu Kaze, amesema ni mapema kulizungumzia suala la kocha huyo kwa sababu liko kwenye kamati ya mashindano wanalifanyia kazi ikiwamo suala zima la maboresho ya timu yao katika kila sekta.
Kikosi cha Namungo FC kimeweka kambi Karatu, Arusha na kitacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Singida Fountain Gate FC, mchezo utakaopigwa leo Jumatatu (Julai 24), mkoani humo.
Kikiwa huko kitacheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kurejea Dar es Salaam na kucheza mingine miwili na baada ya hapo kitarudi maskani kwao, Ruangwa, Lindi tayari kwa kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 15, mwaka huu.