Kocha Mkuu wa Namungo FC, Cedric Kaze baada ya kuiongoza timu yake kwa mechi tano akikusanya Pointi tatu na kupoteza kumi amesema mchezo dhidi ya Singida Big Stars umeshikilia hatma yake, hivyo anahitaji Pointi tatu.
Namungo FC kwenye mechi tano ilizocheza imepoteza mbili na kutoka sare tatu ikianza na Kagera Sugar (1-1), Mashujaa (0-0), Young Africans (1-0), KMC FC (1-1) na walikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania.
Kaze ambaye ni kocha wa zamani wa Young Africans amesema anaingia kwenye mchezo dhidi ya Singida BS akiwa na uhitaji wa Pointi tatu muhimu kwa lengo la kujihakikishia kibarua chake ndani ya timu hiyo.
Hautokuwa mchezo rahisi tunakutana na timu ambayo pia inapambana kukusanya Pointi tatu, hivyo dakika 90 bora ndio zitaamua matokeo,” amesema kocha huyo raia wa Burundi aliyewahi kufanya kazi kwenye akademi za Barcelona, Hispania.
Kaze amesema anatambua umuhimu wa Pointi hizo, mbali na kibarua chake kuwa rehani anatakiwa kujitengenezea CV nzuri ambayo itambeba katika majukumu yake nje ya Namungo FC ambayo pia amekiri kuipambania.
Namungo FC itakuwa nyumbani kuikaribisha Singida Big Stars, Jumamosi ijayo huku siku hiyo kukiwa na mechi nyingine kati ya Geita na Dodoma Jiji, Ihefu na Coastal Union.