Kocha Msaidizi wa Young Africans, Cedric Kaze ameibuka na kutoa kauli moja ya kibabe kwa kusema kuwa hawana wasiwasi tena juu ya wapinzani wao katika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Marumo Gallants ya Afrika Kusini baada ya kupata muda wa kutosha kuwaangalia katika mchezo wao dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Kaze ametoa kauli hiyo kuelekea katika mchezo huo unaotarajia kupigwa kesho Jumatano (Mei 10) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Mei 17, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Marumo ambao kwa sasa wanapambana kubakia katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini kutokana na kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja licha ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Jumamosi (Mei 06) ilikubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Thohoyandou.
Kaze amesema kuwa wamepata muda wa kutosha wakuwasoma wapinzani wao katika mchezo wao muhimu waliokubali kipigo cha mabao 2-0 hali inayowapa matumaini makubwa ya kuweza kufanikiwa kupata ushindi wa kwenda katika hatua ya Fainali ya michuano hiyo.
“Nadhani tuna nafasi kubwa ya kumaliza mchezo hapa nyumbani kwa sababu tumepata muda kuwaangalia katika mchezo wao mkubwa wa ligi ambao waliweza kupoteza, hii imetusaidia kupunguza presha lakini tumeweza kuona mapungufu yao yapo katika nafasi zipi ambazo zinaweza kutusaidia kupata ushindi.”
“Ukweli wapinzani siyo wabaya na hatupaswi kuwadharau kutokana na nafasi waliopo kwenye ligi ya kwao kwa sababu ligi haina mtoano kama katika hii michuano ya CAF.”
“Kikubwa tunaenda kucheza nao tukiwa hatuna presha kwa sababu tunajua tunaenda kucheza na mpinzani wa aina gani na yupo katika wakati gani lakini tunachoweza kukiangalia upande wetu ni kutafuta matokeo ya ushindi,” amesema Kaze