Kuimarika kwa kikosi cha Geita Gold FC kuwamelishtua Benchi la Ufundi la Young Africans, kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa 17 wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaozikutanisha timu hizo Jumapili (Machi 06) katika Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Geita Gold FC watautumia Uwanja wa CCM Kirumba kama Uwanja wao wa nyumbani kufuatia tahadhari za kiusalama walizozichukua kwa kuepusha purukushani ambazo huenda zingejitokeza endapo wangeutumia Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Young Africans.
Kocha Msaidizi wa Young Africans Cedric Kaze amezungumza kwa niaba ya Benchi la ufundi la klabu hiyo kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambapo amesema wanakwenda kuikabili Geita Gold FC kwa tahadhari kubwa kwa sababu tayari wamepata taarifa zote kuhusu kuimarika kwa wapinzani chao tangu mwezi Januari.
Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema wanafahamu Geita Gold ni moja ya timu nzuri zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara huku ikiwa na baadhi ya wachezaji wenye uzoefu, hivyo watalazimika kuongeza umakini katika mchezo huo wa Jumapili.
“Tumesafiri salama na tutakamilisha maandalizi ya mchezo huu tukiwa hapa Mwanza, mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Geita Gold inafanya vizuri katika ligi hivi sasa, wamepata matokeo mazuri kwenye michezo minne ama mitano iliopita.”
“Wameimarika, wamejijenga na kupata wachezaji wazuri katika kipindi cha dirisha dogo, kwa hiyo tunajua hilo, lakini lengo letu ni pointi tatu, tutakwenda kwa tahadhari,” amesema Kocha Kaze baada ya kuwasili jijini Mwanza.
Katika mchezo wa Duru la Kwanza la Ligi Kuu msimu huu uliozikutanisha timu hizo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Young Africans ilichomoza na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Kiungo Mshambuliaji Jesus Moloko.
Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 42, huku Geita Gold FC yenye matokeo ya mazuri kwa siku za karibuni ikiwa na alama 21 zinazoiweka katika nafasi ya 07 kwenye msimamo.