Kocha Msaidizi wa Young Africans Cedrick Kaze amesema haikuwa dhamira yake kumaliza mchezo dhidi ya Ruvu Shooting kwa kupata matokeo ya sare ya bila kufungana jana Jumatano (Mei 04), Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Kaze ambaye anakaimu nafasi ya Kocha Mkuu Nesreddine Nabi aliyekua anatumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu, amesema dhumuni kubwa katika mchezo huo lilikua ni kuondoka na matokeo mazuri, lakini mambo yaliwaendea tofauti.
Amesema alijitahidi kutumia mbinu zote ili kufanikisha mpango wa kuifunga Ruvu Shooting, lakini uimara wa timu pinzani ulikua kikwazo, licha ya safu yake ya ushambuliaji kujaribu mara kwa mara kupata bao.
“Halikua kusudio letu kuja hapa na kupata alama moja, tulidhamiria kupata alama zote tatu, ila mambo yamekua tofauti, hivyo hatuna budi kukubali tulichokipata kutoka kwa wenzetu.”
“Nilijaribu mbinu tofauti ambazo huenda zingefanikisha lengo la kupata matokeo mazuri tukiwa hapa Kigoma, lakini bado ninasisitiza matokeo haya tulioyapata ni sehemu ya mchezo na tumeyapokea.” amesema Kaze
Katika hatua nyingine Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema Benchi la Ufundi la Young Africans limetambua madhaifu yaliyojitokeza na kupelekea matokeo ya sare katika michezo miwili mfululizo, hivyo wamejizatiti kuyafanyia kazi ili kurudi katika njia ya ushindi.
“Kama Benchi la Ufundi tumeona mapungufu kadhaa, tutayafanyia kazi katika mazoezi yetu ili tuweze kufanya vizuri katika mchezo wetu ujao, ninaamini tutafanya vizuri.” ameongeza Kaze
Pamoja na kuondoka na alama moja mkoni Kigoma, Young Africans inaendelea kuwa kileleni mwa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha alama 56, huku Ruvu Shooting ikiwa na alama 22 zinazoiweka nafasi 13.