Kocha kutoka nchini Burundi Cedrick Kaze anapewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Fredy Felix Minziro aliiyetupiwa virago Geita Gold FC, baada ya mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu 2022/23.
Kaze anatajwa kuwa katika mipango ya Geita Gold FC, kufautia mkataba wake na Young Africans kumalizia na sasa yupo huru kujiunga na klabu yoyote ya ndani na nje ya Tanzania.
Mmoja wa viongozi wa Geita Gold FC, amesema kuna asilimia kubwa ya Kaze kupewa jukumu la kuwa Kocha Mkuu ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa sababu ya mafanikio waliyoyapata Young Africans kwa msimu uliomalizika wa 2022/23.
“Kaze ndio jina ambalo liko mezani kwa viongozi na kutajwa sana kuwa atakuja kuchukuwa nafasi ya Minziro, hadi sasa kocha huyo bado hajasaini mkataba mwingine na Young Africans, uongozi utapeleka ofa kwake na kuona uwezekano wa kuwa naye msimu ujao,” amesema kiongozi huyo.
Amesema kuna maboresho ambayo uongozi wa klabu hiyo umepanga kuyafanya kabla ya kuanza msimu mpya na maeneo wanayoyaangazia ni kuwa na benchi bora la ufundi pamoja na kuongeza wachezaji wengine wenye ubora.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Leonard Bugomora amesema “Kwa sasa siwezi kumzungumzia jambo lolote kwa sababu nipo katika majukumu makubwa, labda muwasiliane na Katibu wetu,”
Geita Gold FC ilimaliza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2022/23 ikishika nafasi ya saba, huku Uongozi wa klabu hiyo ukidhamiria kufanya makubwa katika Ligi hiyo msimu ujao 2023/24, ambao umepangwa kuanza kati ya mwezi Agosti au Septemba.