Kocha Cedrick Kaze leo Jumatano (Septemba 20) ana kibarua cha kumfunga paka kengele wakati timu yake ya Namungo FC itakapokuwa ugenini dhidi ya Young Africans katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam kuanzia saa 1:00 usiku.
Mtihani huo mgumu kwa Kaze ni wa kuvunja mwiko wa Young Africans kutopoteza mchezo au kuruhusu bao katika dakika 90 za kawaida za mechi ya mashindano ambapo hadi sasa timu sita zimeushindwa tangu msimu huu ulipoanza.
Timu hizo ambazo hakuna hata moja iliyoweza kupata ushindi au kufunga bao katika dakika 90 dhidi ya Young Africans ni Azam FC, Simba SC, KMC, JKT Tanzania, ASAS ya Djibouti na Al Merrikh ya Sudan.
Kaze ambaye alijiunga na Namungo FC msimu huu akitokea Young Africans, mbali na kibarua hicho, pia ana kazi ya kuiongoza Namungo FC kuhitimisha unyonge ilionao dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, kwani tangu ilipopanda daraja haijawahi kushinda katika mechi saba za ligi baina yao ambapo Young Africans imeibuka na ushindi mara mbili na zimetoka sare tano.
Wakati wenyeji Young Africans wakiingia na takwimu bora za kushinda mechi zao mbili zilizopita za ligi dhidi ya KMC na JKT Tanzania ambazo walishinda mabao 5-0 katika kila mchezo, Namungo FC wenyewe hawajaanza vizuri ambapo katika mechi mbili dhidi ya timu hizo hizo zilizocheza na Young Africans wametoka sare moja na kufungwa moja.
Kocha mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi alisema jana Jumanne (Septemba 19) kuwa katika mchezo huo anaweza kuwa na mabadiliko ya kikosi kitakachoanza.
“Siwezi kuwadharau wapinzani wangu kwa sababu nimewaangalia mechi mbili za nyuma na nimeona sio timu mbaya kabisa bali wanacheza vizuri.
Tunaweza kuwa na mabadiliko kidogo kwenye kikosi changu katika mchezo huu na lengo ni kutoa nafasi kwa wachezaji wengine ndani ya timu yangu,” alisema Gamondi.
Gamondi aliongeza akisema: “Kazi kubwa ya washambuliaji wake ni kuhakikisha wanafunga tu kwa sababu hiyo ndio kazi kubwa.”
Kaze kwa upande wake alisema Namungo walikuwa na muda wa takribani mwezi mmoja kujiandaa kwa ajili ya mchezo huo.
“Tunajua Young Africans ina rekodi nzuri msimu huu kwa kufunga mabao matano katika mechi mbili zote huku ikiwa haijaruhusu bao. Hiyo kwetu ni hamasa kuhakikisha tunafanya vizuri.
“Wachezaji wangu nao ni sehemu ya kuonyesha uwezo na tutafanya kila kitu tuonyeshe uwezo wetu,” alisema Kaze.