Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, imetangaza rasmi wagombea 24 waliojisajili kwa uchaguzi wa Rais utakaofanyika Desemba 20, 2023 ambapo orodha kamili ya wagombea itachapishwa Novemba 18, 2023 siku moja kabla ya kuanza rasmi kwa Kampeni za uchaguzi.
Miongoni mwa wagombea waliojisajili ni pamoja na Rais wa sasa, Félix Tshisekedi, ambaye amekuwa madarakani tangu Januari 2019 na anawania muhula mpya wa miaka mitano.
Upande wa upinzani, kuna wagombea wenye ushawishi mkubwa akiwrmo Dkt. Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2018, Moïse Katumbi, mfanyabiashara tajiri na aliyekuwa Gavana wa Katanga na Martin Fayulu, ambaye ni mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa Rais wa 2018, ambao anadai kuwa alishinda.
Mwingine ni Mbunge Delly Sesanga na Mawaziri Wakuu wa zamani Adolphe Muzito na Augustin Matata Ponyo, huku swali kuu likiwa ni iwapo upinzani uliogawanyika utaweza kukubaliana kutoa mgombea mmoja.
Dk. Denis Mukwege
Kati ya wagombea 24 waliosajiliwa, mmoja pekee ni mwanamke, Marie-Josée Ifoku Mputa, ambaye tayari alikuwa mgombea katika uchaguzi wa Rais wa Desemba 2018, ambapo CENI iliandikisha wagombea 21 katika uchaguzi huo wa Rais utakaombatana na uchaguzi wa Bunge, Mikoa na wa Manispaa.
Marie-Josée Ifoku Mputa
Hata hivyo, hali ya kisiasa imekuwa tete kwa miezi kadhaa, huku vyama vya upinzani vikilaumu kupungua kwa nafasi ya kidemokrasia na kueleza uhakika wao kuwa uchaguzi utaguswa na udanganyifu.