Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Imani Kajula, ameahidi kusuka timu tishio ambayo anaamini itakwenda kufuzu hatua ya Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Brani Afrika msimu ujao 2023/24.
Kajula amesema Simba SC imejifunza mambo mengi kupitia Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23, licha ya kushindwa kufikia lengo la kucheza Nusu Fainali.
Simba SC ilikuwa klabu pekee ya Afrika Mashariki iliyotinga Robo Fainali ya Michuano hiyo, na baade kutolewa na Mabingwa watetezi Wydad AC, iliyokuwa nyumbani mjini Casablanca nchini Morocco kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati.
Kajula amesema: “Niseme tu, mpira wa Tanzania unapiga hatua kubwa Afrika, tumeondoka Morocco, kila mtu anaisifu Simba SC na kila mtu anasifu mpira wa Tanzania, lakini hili lisitufanye tukabweteka, ila tulione kama ni changamoto ya kufanya vema zaidi.”
“Na sisi kama klabu hilo ndilo lengo letu, hii ni sehemu ya kujipimia na ninavyokwambia tunakwenda kusuka kikosi zaidi ili tuje kushindana vizuri zaidi kipindi kijacho.”
“Uzuri ni kwamba michuano ya Super Cup inaanza wakati wa msimu mpya wa ligi na michuano mingine, kwa hiyo tuna ripoti ya mwalimu, wataalam wachambuzi na waangalizi wa soka kwa ajili ya kuboresho kikosi, na tumeona kuna maeneo ya kuyafanyia kazi na tutayafanyia kazi kweli bila matatizo yoyote,”
Wakati huo huo Kiungo kutoka Zambia Clatous Chama amesema walipambana kiasi cha kutosha kwa ajili ya mashabiki, wanachama na familia zao, lakini haikuwa bahati yao.
“Hatuna cha kusema, kweli tumetoka, lakini mimi nashukuru kwa Mungu, viongozi wetu. mashabiki, familia na wote waliokuwa wanatupa sapoti, lakini mimi naona kama tumepambana vizuri tu, haikuwa bahati yetu ni mipango ya Mungu tu, tumshukuru Mungu.
“Kukosa penalti inaumiza sana, lakini ni mpira hatuwezi kusema mengi na imepita, tutaangalia yale yanayokuja mbele,” amesema Chama