Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC Iman Kajula amesema Wachezaji wa klabu hiyo wamekuwa wakilipwa Posho zao kwa wakati na hadi sasa wameshawalipa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.1.
Jana Jumanne (Mei 09) Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally alikiri Wachezaji wanadai sehemu ya fedha za Posho, lakini akaahidi watalipwa, na suala hilo sio kikwazo kwao kufanikisha matokeo ya Uwanjani hasa katika kipindi hiki ambacho wameshindwa kuwa sehemu ya timu zinazowania Ubingwa wa ndani na nje ya Tanzania.
Imani Kajula amesema Fedha za Posho kwa wachezaji wanazodai ni za michezo ya ndani, lakini upande wa Kimataifa wameshalipwa.
Hata hivyo kiongozi huyo aliyechukua nafasi ya Barbara Gonzalez aliyeondoka mwanzoni mwa mwaka huu, amesema inashangaza kusikia baadhi ya wadau wanalipigia kelele suala hilo, wakati Uongozi umefanikisha kulipa zaidi ya Bilioni 1, hivyo hauwezi kushindwa kulipa shilingi Milion 20 zilizobaki.
“Timu yetu imeshatoa Bonus zaidi ya Billion 1.1 na kiasi kilichobaki ni milioni 20 pekee tena ni Bonus ya Ligi ya ndani, wewe vuta picha Klabu inalipa zaidi ya Billion 1.1 inashindwaje kulipa milioni 20, haingii akilini hilo ni jambo linalopitia mchakato wa kitaasisi na lipo ndani ya uwezo wetu.”
“Vuta picha wachezaji wanalipwa mshahara kiasi gani na ukilinganisha na milioni 20 ambayo watagawana watu zaidi ya 30, kila mmoja atapata kiasi gani, ambapo kukosekana kwake ije iathiri matokeo kwenye mechi.”
“Kwenye mikataba yao hakuna sehemu ambayo imesema itawalipa Bonus, ila huwa wanatoa kwa ajili ya kuwahamasisha wapambane zaidi kwenye kile wanachokipambania.” Amesema Kajula
Sakata la kutolipwa sehemu ya Posho kwa wachezaji Simba SC liliibuka baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa Nusu Fainali na kutolewa katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kufungwa 2-1 na Azam FC mkoani Mtwara Jumapili (Mei 07).
Kwa sasa Simba SC ina kazi ya kumalizia michezo mitatu ya Ligi Kuu iliyosalia dhidi ya Ruvu Shooting, Coastal Union na Polisi Tanzania ili kutamatisha msimu wa 2022/23, ambao unashuhudia wakiondoka mikono mitupu.