Beki wa pembeni kutoka nchini Hispania na klabu ya Chelsea Cesar Azpilicueta amesema hata ikitokea wawachukua ubingwa wa kombe la chama cha soka England (FA CUP) haitowasaidia kuficha mapungufu waliyonayo msimu huu.
Azpilicueta alisema maneno hayo dakika chahe baada ya mchezo wao ligi dhidi ya West Ham Utd, uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja na kuifanya klabu hiyo ya Magharibi mwa jijini London kuwa nyuma kwa poiny 10 dhidi ya Liverpool na Tottenham.
Chelsea ambao ni mabingwa watetezi nchini England, wamekua na msimu mbaya na wana kila dalili za kushindwa kucheza michuano ya ligi ya mbingwa barani Ulaya msimu ujao.
“Tukubali hatujafanya vizuri msimu huu, na halitokua jambo la busara kujidaia ubingwa wa FA endapo tutafanikiwa kuuchukua mwezi ujao,” amesema Azpilicueta.
“Kombe la FA lina hadhi yake hapa England, lakini bado ninasisitiza haitopendeza kuficha udhaifu wetu kwenye michuano hiyo ambayo bado ipo wazi kwa klabu nyingine ambazo zimeingia katika hatua ya nusu fainali.” Aliongeza beki huyo mwenye umri wa miaka 28.
Chelsea watacheza dhidi ya Southampton hatua ya nusu fainali ya kombe la FA April 22, huku Man utd wakipangwa kukutana na Tottenham Hotspur.
Katika upande wa ligi kuu, Chelsea wamebakisha michezo sita ambayo kimahesabu kama watashinda yote watafanikiwa kufiki lengo, endapo wapinzani wao katika harakati za kuwania nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao Liverpool na Tottenham watapoteza michezo yao mitano iliyosalia kwa kila mmoja.
Michezo iliyosalia ya ligi kwa upande wa Chelsea itakua dhidi ya Southampton mwishoni mwa juma hili (Jumapili), kisha Burnley (April 19), Swansea City (April 28), Liverpool (Mei 06), Huddersfield Town (Mei 09) na Newcastle United (Mei 13).