Beki wa Pembeni na Nahodha wa kikosi cha Chelsea Cesar Azpilicueta anakaribia kuhamia klabu ya Inter Milan, baada ya kukubali maslahi binafsi na uongozi wa klabu hiyo Italia inayoshiriki Ligi ya Serie A.

Mchezaji huyo anayependwa na mashabiki wengi amekuwa hana namba mbele ya Reece James na alikaribia kuondoka Chelsea mwaka jana huku FC Barcelona ikihusishwa na kutaka kumsajili.

Wakati Beki Malo Gusto, akitarajiwa kutuwa Stamford Bridge msimu huu wa majira ya joto ili kutoa ushindani zaidi kwa James, Azpilicueta ameambiwa yuko huru kuondoka Chelsea na vyanzo vimethibitisha anakaribia kuhamia Inter.

Azpilicueta mwenye umri wa miaka 33, amezungumza na FC Bayern Munich na pia akapokea ofa kutoka Saudi Arabia, lakini anatazamiwa kupeleka kipaji chake Inter Milan na anatajwa kupewa miaka miwili.

Licha ya kuwa bado ana mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Chelsea, Azpilicueta anatarajiwa kuruhusiwa kuhama kama ishara ya heshima kwa miaka 11 ya utumishi wake.

Azpilicueta alijiunga na Chelsea kutoka Marseille mwaka 2012, lakini hivi karibuni alijiimarisha kama sehemu muhimu ya safu ya ulinzi ya Chelsea, akicheza kulia na kushoto na hata kubadilika kuwa beki wa kati baadaye katika maisha yake ya soka.

Hadi anahusishwa kuondoka Chelsea, Azpilicueta amecheza mechi 508, na kumfanya awe nafasi ya sita kwenye orodha ya wachezaji bora wa muda wote wa klabu hiyo.

Chelsea na Inter wamekuwa kwenye mazungumzo katika msimu mzima wa majira ya joto kuhusu masuala mbalimbali.

Wakati ‘The Blues’ wameachana na mpango wa kumnunua mlinda mlango Andre Onana, mazungumzo bado yanaendelea kuhusu mshambuliaji Romelu Lukaku.

Josko Gvardiol anawindwa mitaa ya Manchester
Mkude afunguka ishu ya Young Africans