Kwa mara ya kwanza kiungo wa Chelsea Cesc Fabregas amekiri kujihisi vibaya kuhusu mpango wa kuwekwa benchi mara kwa mara na meneja wa sasa wa klabu hiyo Antonio Conte.
Fabregas alikua anaficha hisia zake kuhusu suala hilo kila alipoulizwa na waandishi wa habari, lakini kwa sasa ameonyesha kuchoshwa na maamuzi ya Conte na Kusema yanamsikitisha.
Fabregas amekua akihaha kurejea katika kikosi cha kwanza tangu mwanzoni mwa msimu huu, na wakati mwingine alifikia hatua ya kuhusishwa na mpango wa kuuzwa, kwa kudaiwa hayupo kwenye mipango ya Antonio Conte.
“Ninacheza soka ili nishinde na nijihisi furaha. Inapotokea sichezi ninajihisi vibaya na huwa sifurahishwi na hali hiyo, japo ninajivunia kuwa sehemu ya wachezaji wa klabu ya Chelsea.” Fabregas aliiambia tovuti ya Chelsea.
“Soka ni mchezo wa maisha yangu, ni kila kitu kwangu. Wakati wote ninapenda kuwa sehemu ya uwanja ili nidhihirishe uwezo wangu.”
Fabregas alisajiliwa na Chelsea mwaka 2014 wakati wa utawala wa Jose Mourinho, akitokea FC Barcelona na mpaka sasa ameshaitumikia The Blues katika michezo 81 na kufunga mabao 9.